Katiba mpya: 'tuko tayari wote kuwekwa ndani, asema Kiongozi wa Upinzani Tanzania Mbowe

 


Chama kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA kimesema hakitaendelea kumpigia magoti Rais wa nchi hiyo, Samia Hassan Suluhu kuhusu mustakabali wa taifa hilo.

Mwenyekititi wa CHADEMA, Freeman Mbowe amewaambia waandishi wa habari hayo leo, kufuatia Jeshi la Polisi la nchi hiyo kuwakamata viongozi, wanachama wa chama hicho pamoja na viongozi wa dini 38 waliokuwa wahudhurie mkutano wa chama hicho kupitia baraza lake la vijana (BAVICHA) wenye lengo la kuhamasisha kupatikana kwa katiba mpya ya nchi hiyo.

Mara baada ya kuingia madarakani mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia alitangazia umma dhamira yake ya kukutana na wapinzani ili kuzungumzia maswala mbalimbali ikiwemo ya kisiasa na namna gani ya kuendesha shughuli za siasa. Licha ya kukutana na makundi mengine kama vijana, wazee na wanawake mpaka sasa Rais Samia hajakutaa na wapinzani.

‘‘Hatuwezi kuendelea na ule utaratibu wa zamani, tuna haki ya kukutana tunakamatwa, tunapigwa, tunashitakiwa, tunasoteshwa mahakamani miaka miwili miaka mitatu, kisha tunaachiwa huru, ama tunahukumiwa vifungo batili tukikata rufaa sote tunashinda’, alisema Mbowe

Pamoja Polisi kuzuia mkutano huo uliokua ufanyika kwenye ukumbi wa Hotel ya Boma wiki hii na kukamata watu hao 38, Kiongozi huyo wa Upinzani amesema, mkutano upo pale pale na utafanyika wiki hii na kama kukamatwa wako tayari kukamatwa wote.

‘Kama wanataka kuwaweka ndani wanachadema kwenye hoja hii ya katiba, wapanue kwanza na magereza, kwa sababu tuko tayari wote tuwekwe ndani , na wala hatutaomba dhamana’ alisema Mbowe kabla ya kulaani kitendo cha Jeshi la Polisi Mwanza, kuwakamata viongozi wa dini na wafuasi wa chama hicho

Kwa zaidi ya miaka mitano sasa tangu utawala wa Rais John Magufuli na sasa utawala wa Rais Samia mikutano ya kisiasa imezuiliwa kufanyika nchini humo, hatua inayopingwa vikali na upinzani wanaosema, katiba inaruhusu mikusanyiko na sheria za nchi zinaruhusu mikutano hiyo ya kisiasa kufanyika.

Mbowe amesema kama Chama na wananchi wa Tanzania wana haki ya kukutana kwa mujibu wa sheria, hivyo chama chake kitafanya mkutano wa juu wa Baraza kuu la chama Julai 31 mwaka huu ili kutoa baraka ya kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.

‘Ni haki yetu kukutana, tutahama kutoka mikutano ya hadhara na sasa tutaingia kuandamana. Tunamwambia mama Samia Suluhu, akizidi kuchelewesha jambo hili, anazidi kuleta mpasuko katika nchi hii, anavyolichelewesha anachelewesha kuwaunganisha Watanzaia, tujenge taifa moja la watu wanaopenda na kuheshimiana’, alisema Mbowe

Alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, kuhusu masuala ya katiba mpya na na mikutano ya hadhara Rais Samia alisema kwanza apewe muda wa kujenga uchumi na kufungua nchi kabla ya kuruhusu mikutano hiyo na masuala mengine ya kisiasa.

Comments