Al Shabaab: Wanawake waislamu waliwafunika Hijab wakristo



Mwalimu mmoja aliyenusurika kifo katika shambulizi la basi lililotekelezwa na wapiganaji wa Al shabaab hapo jana ameiambia BBC kuwa wanawake wa Kiislamu walivua hijab na kuwastiri wanawake wakristu ilikuwaokoa wasiuawe.
Mwalimu huyo ambaye ni mmoja wa abiria wa basi hilo la umma waliojeruhiwa wakati wa shambulizi hilo la alfajiri anasema punde baada ya basi hilo kutekwa, Magaidi hao waliwaeleza kuwa waislamu wote wako salama.
''Walituambia kuwa sisi waislamu tulikuwa salama na hivyo tukang'amua kuwa wanawalenga wakristu''
''Hapo ndipo wanawake wakavua hijab zao na kuwastiri wanawake wakristo''.
''Kwa sababu walikuwa ni wanaume ,wanawake walijitenga na kuwaficha wanawake wakristo na hivyo kuwaokoa wasiuawe'' alisema mwalimu huyo ambaye anauguza majeraha mjini Mandera.


'Ilikuwa vigumu kutambua nani ni muislamu na nani siye''
Idadi ya wahasiri ilikuwa ndogo kufuatia jitihada za abiria waislamu kuwaficha na kuwaokoa wenzao wakristo waliokuwa wakisafiri pamoja.
Tukio hilo limevutia hisia kali kote duniani.
Mwezi Novemba mwaka uliopita wapiganaji wa Al Shabaab waliteka basi moja na kuwaua abiria 28 ambao hawakuwa Waislamu.
Kundi hilo liligonga vichwa vya habari mwezi Aprili lilipowaua wanafunzi wakristo 148 katika chuo kikuu cha Garissa.

Comments