Wizara ya Afya ya Rwanda jana ilitangaza habari ya kugunduliwa wagonjwa 964 wapya wa corona au COVID-19 kutoka sampuli 8,741 za watu waliochukuliwa vipimo ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kuripotiwa kwa siku moja tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kwa mara ya kwanza nchini Rwanda mwezi Machi 2020.
Wizara hiyo ya afya ya Rwanda imeongeza kuwa, idadi hiyo ya wagonjwa waliopatikana kutoka kwenye vipimo hivyo 8,741, inaunda asilimia 11.2 ya vipimo hivyo.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, jana Jumatano ilikuwa ni siku ya tatu mfululizo kuvunja rekodi idadi ya wagonjwa wa corona nchini humo. Idadi ya jana ya wagonjwa 964 ni ya kwanza kuwahi kuripotiwa nchini humo kwa siku moja.
Taarifa ya Wizara ya Afya ya Rwanda imesema pia kuwa, wagonjwa wengine watano wamefariki dunia kwa corona na kufanya idadi yote ya wagonjwa waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo huko Rwanda kufikia 397
Vyombo vya habari vimelinukuu gezeti la kila siku la The New Times la serikali ya Rwanda likisema kuwa, watu 33,260 wameshathibitishwa kukumbwa na ugonjwa wa corona nchini humo kutoka zaidi ya vipimo milioni moja na laki tano na 70,000 vilivyochukuliwa hadi hivi sasa. Zaidi ya wagonjwa 26,734 wameshapata afueni kutokana na ugonjwa huo na kuruhusiwa kurudi makwao.
Wagonjwa wa corona waliopo hivi sasa nchini Rwanda ni zaidi ya 6,129 kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Rwanda ni katika nchi zilizofanikiwa sana kudhibiti ugonjwa wa corona au COVID-19.
Kwa mujibu wa "Africanews," mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, Rwanda ilikuwa miongoni mwa nchi kuu Afrika zilizodhibiti vizuri ugonjwa wa COVID-19.
Comments
Post a Comment