Mkutano maalum wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaendelea mjini Geneva kujadili hali nchini Burundi.
Kabla
ya mkutano huo kufanyika mjini Geneva, Uswizi, Katibu Mkuu wa umoja UN
Ban Ki-moon alikuwa ameonya kuwa taifa hilo limo hatarini ya kutumbukia
kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yanaweza kuathiri kanda
yote.Amesema machafuko yaliyotokea nchini Burundi siku za hivi majuzi “yanaogofya” na kwamba atamtuma mshauri wake maalum kwenda Burundi kwa mashauriano ya dharura na serikali.
Balozi wa Marekani katika UN Samantha Power amesema umoja huo umechelewa kuchukua hatua kuhusu mzozo huo.
Kamishna wa UN kuhusu haki za binadamu Zeid Ra'ad al Hussein, akizungumza katika mkutano huo, amekariri matamshi ya Bw Ban.
Amenukuliwa na Reuters akisema: “Burundi imo katika njia panda na inaweza kukabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.”
Ameomba hatua madhubuti zichukuliwe na jamii ya kimataifa, zikiwemo kutolewa kwa marufuku za kutosafiri kwa wahusika pamoja na kuzuiliwa kwa mali.
Mkutano huo maalum umefanyika kufuatia ombi la Marekani.
Kabla ya mkutano maalum kama huo kufanyika, unahitaji kuidhinishwa na theluthi ya mataifa wanachama wa baraza hilo la umoja huo, ambayo ni mataifa 16, jambo ambalo tayari limefanyika, Ghana ikiwa miongoni mwa nchi zilizoidhinisha ombi hilo.
Mara ya mwisho mkutano maalum wa baraza hilo kufanyika ilikuwa 1 Aprili 2015, ambao ulijadili mashambulio ya kigaidi yaliyokuwa yakitekelezwa na kundi la Boko Haram.
Comments
Post a Comment