January Makamba aanza kuitikisa CCM......Ni kuhusu kauli yake ya Rais Kijana 2015....Yadaiwa anawza kusababisha mpasuko
- Get link
- X
- Other Apps
KAULI iliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Bw. January Makamba, akidai Tanzania kwa sasa inahitaji Rais kijana, imeanza kuibua maswali kwa baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Shinyanga.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Bw. Charles Shigino, alisema kauli ya Bw. Makamba aliyoitoa akiwa nchini Uingereza inaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM kwa vile inaonesha ubaguzi wa wazi kwa baadhi ya wanachama wake.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga jana, Bw. Shigino alisema yeye binafsi anailaani kauli hiyo ambayo ameifananisha na siasa za ubaguzi ndani ya chama ili kulibagua kundi moja la wanachama.
Alisema CCM, imekuwa ikipinga suala la ubaguzi wa aina yoyote hivyo kauli ya Bw. Makamba kutaka Rais ajaye mwaka 2015 awe kijana inaweza kusababisha mpasuko kwani inapingana na Katiba ya CCM.
“Makamba anapaswa kuelewa kuwa, ujana si kigezo cha kuwa na sifa za kugombea nafasi ya urais, nafasi hii ni nyeti na mtu anayechaguliwa anapaswa kuwa na busara, uwezo wa kuongoza nchi bila kuyumba.
“Wapo wazee wenye sifa hizi kuliko vijana...kauli hii pia inapingana na Katiba ya chama chetu labda paitishwe Mkutano Mkuu tuweze kufanya mabadiliko ya Katiba vinginevyo hoja ya ndugu yetu haitakuwa na mashiko kama wazee watajitokeza kuwania urais,” alisema.
Aliongeza kuwa; “Katiba ya CCM Ibara ya 14 vifungu vidogo vya (1) hadi (3), vinafafanua wazi juu ya haki za mwanachama ikiwemo ya kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi, hapa haijataja wenye haki hiyo ni vijana tu, inawezekana Makamba,” alifafanua Shigino.
Alisema ni vizuri Bw. Makamba akajifunza kutoka kwa wazee waasisi wa taifa hili ambao waliwahi kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa badala ya kutoa kauli zinazoashiria mianya ya ubaguzi ndani ya CCM hivyo kuhatarisha mstakabali wa chama katika chaguzi zijazo.
“CCM ni chama kikongwe nchini, ndani yake kuna akina mama, wazee na vijana ambao wote wana haki sawa kwa mujibu wa katiba yetu, mimi sioni tatizo la mgombea urais kwa tiketi ya CCM atokane na vijana au wazee, wote ni sawa, mradi wawe na sifa, vigezo vinavyohitajika,” alisema.
Shigino aliviomba vikao mbalimbali vya uteuzi ndani ya CCM, kuipuuza kauli ya Bw. Makamba na wajumbe wake wasiwe tayari kuongozwa na matakwa ya watu, bali wazingatie katiba na kanuni za chama katika uteuzi wao na muhimu kuangalia mtu gani mwenye uwezo wa kuivusha CCM 2015 bila kujali ni mzee au kijana
Comments
Post a Comment