Viungo vya binadamu vyatupwa jalalani MUHIMBILI..... Kunguru, paka wafanya sherehe, harufu mbaya yatanda
Hospitali ya Taifa
Muhimbili, inalazimika kutupa taka za hospitali jalalani vikiwamo viungo vya
binadamu vilivyokatwa baada ya kukosekana kwa tanuru la kuchomea taka
(insinereta) kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.
Kitendo hicho
kinasababisha taka hizo kutoa harufu kali huku paka na kunguru wakichangamkia
kufukua baadhi ya viungo hivyo vilivyotupa na kuvitawanya ovyo.
Baadhi ya wafanyakazi
wa hospitali hiyo waliiambia NIPASHE kuwa tanuru hilo limeharibika zaidi ya
miezi mitatu, huku kampuni ya K Environment iliyokuwa na zabuni ya kuzoa taka
hizo, ikidaiwa kukatisha mkataba baada ya kutoelewana kwenye taratibu za malipo.
Walidai kuwa hospitali imekuwa ikizikusanya taka hizo na kuzichoma nyakati za
usiku.
Nipashe lilishuhudia
mlundikano wa taka karibu na wodi ya wazazi ndani ya shimo lililokuwa
limechimbwa kwenye eneo lililo karibu na nyumba za wauguzi na madaktari.
Watumishi hao
walidokeza kuwa uchomaji wa taka hizo hufanywa usiku hivyo kujaza moshi na
harufu karibu na nyumba zao.
Mmoja wa madaktari
hospitali hapo ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema: “uchomaji huo
wa mabaki ya binadamu pamoja na sindano na dawa sio salama.
“Kitaalamu ili sindano
iungue na kuyeyuka huhitaji nyuzi joto zaidi ya 100 nashangaa uchomaji
unaofanyika hapa.”
Tanuru lililoharibika
ukarabati wake zahitajika Sh.milioni 22.3 tu
Alisema tanuru hilo
lilianza kuleta usumbufu Juni mwaka jana ambapo ukarabati wake ulielezwa
kuhitaji Sh. milioni 22.3.
“Hata baada ya
kufahamu tatizo uongozi wa hospitali ulikuwa unafanya marekebisho madogo madogo
ambayo gharama zilizotumika zinaweza kuzidi fedha ambazo zilitakiwa awali kwa
ajili ya matengenezo.”
KUPUUZA TATIZO
Daktari huyo
alibainisha kuwa tanuru lilipoanza kuwa na matatizo taka hizo zilikuwa
zikipelekwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) kuchomwa na
hospitali ilikuwa inatoa fedha kugharamia kazi hiyo.
“Wakati taka zinazagaa
jalalani, Mkurugenzi wa Muhimbili amenunua gari la anasa aina ya Toyota Land
Cruiser V8 ambalo thamani yake ni zaidi ya Sh. milioni 200,” kilisema chanzo kingine ndani ya ofisi ya
kigogo huyo.
Aidha, chanzo hicho
kimebainisha kuwa, ununuzi wa gari hilo umewashangaza wengi kwa kuwa fedha hizo
zingeelekezwa kwenye kutatua kero mbalimbali zikiwamo vifaa ndani ya hospitali
hiyo.
“Fedha za manunuzi ya
gari hilo ambalo lina mwezi sasa zimepatikana wapi ikiwa zile za kutengeneza
insinereta hazipo? Unanunua V8 wakati hospitali haina hela za kununua betri za
mashine za kupima presha, huu siyo ubinadamu,” kililalamika chanzo chetu na kuongeza:
“Vifaa vya kupimia
joto hizi ‘thermometer’ hakuna, utakuta kwenye wodi moja yenye wagonjwa 70
wanaohudumiwa na wauguzi wawili wananyang’anyana kipimajoto hiyo ndiyo
hospitali kubwa ya rufaa ya taifa...” kimesema.
Baadhi ya wafanyakzi
walihoji jukumu la kitengo cha ubora cha hospitalini hapo kuwa kazi yake ni nini
kama hayo yote yanatendeka.
Baadhi ya wagonjwa
waliofika hospitalini hapo walisema eneo la hospitali lipo kwa usalama wa afya
za wanadamu hivyo uchafu huo ni chanzo cha kuendeleza magonjwa ya kuambukiza.
Walisema kuna chumba
cha upasuaji na oparesheni zinafanyika kila wakati na uchafu uliorundikwa pale
ni wa miili ya binadamu ambao unaliwa na paka na kunguru wanaoweza kubeba
maradhi.
MAELEZO YA HOSPITALI
Mkuu wa Kitengo cha
Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alithibitisha kuharibika kwa tanuru
hilo na kueleza kuwa taka hizo zilikuwa zikipelekwa Muhas kuteketezwa, lakini
mashine ya chuo hicho nayo imeharibika na sasa zinachomewa jalalani.
Alibainisha kuwa taka
hizo zinawekwa kwenye shimo la urefu wa mita mbili hadi tatu na dawa aina ya
‘povidone iodine’ inayoangamiza vimelea vya maradhi, vikiwemo virusi na fungasi
inatumiwa. Pia wakati mwingine dizeli hutumiwa kuzichoma taka hizo.
Aligaesha alisema
utaratibu huo hutumiwa kuzika wanyama waliokufa kwa maradhi ya kuambukiza kama
kipindupindu na kimeta na kwamba hufanywa mbali na vyanzo vya maji.
“Mashine yetu iko
kwenye matengenezo yanayotarajiwa kukamilika wiki ijayo,” alisema na kukanusha kuwa uchomaji
unaofanyika huathiri afya za binadamu kwa vile utaalamu unatumiwa kuua vimelea
vya maradhi.
UNUNUZI WA GARI
Aligaesha alikiri kuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili amenunuliwa gari aina ya Toyota Land Cruiser
V8 yenye thamani ya Sh. milioni 207 na kwamba limenunuliwa kwa sababu kwa miaka
10 mkurugenzi mtendaji hakuwahi kuwa na gari, badala yake alikuwa ameazimwa
gari na Wizara ya Afya.
"Kabla ya
kuazimwa gari hili mkurugenzi alikuwa akitumia pick up hata kwa safari za nje
ya hospitali, ilifikia mahali hata ikitokea safari ya wakuu wa taasisi za afya
kukutana nje ya Dar es Salaam, alikuwa akiomba lifti kwa wenzake," alisema na kutetea kuwa ununuzi wa V8 umefuata
taratibu za kisheria.
MASHINE ZA BP
Aligaesha alisema
kuanzia mwezi Mei mwaka huu, wamepokea mashine 81 za kupimia presha ambazo kati
ya hizo 75 zilitoka bohari ya dawa (MSD) na sita zilikuwa za msaada.
Alibainisha kuwa mashine za MSD zina uwezo
mdogo wa kupima watu wengi lakini pia zinatumiwa kwa muda mfupi na ili kuondoa
tatizo hilo Muhimbili itanunua mashine nyingine zinazo dumu zaidi kutoka nje
DMS

Comments
Post a Comment